KUCHANGIA DAMU HUZUIA MAGONJWA YA MOYO
DAR ES SALAAM
MPANGO wa Taifa wa Damu salama umekiri kukabiliwa na uhaba
wa damu na kusababisha baadhi ya hospitali hapa nchini kuwa na tatizo hilo jambo
ambalo ni hatari miongoni mwa wagonjwa na wahitaji wengine wa huduma hiyo licha
ya kuwapo faida lukuki za kuchangia damu.
Akizungumza na Mwandishi wetu ofisini kwake jijini Dar es salaam mapema wiki
hii, Afisa uhusiano wa mpango huo, Rayah Hamad alisema hali ya damu katika
benki ya mpango huo hairidhishi kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo baadhi ya
watu kuwa na imani potofu, hofu ya kupima damu.
Akifafanua, Hamadi alisema katika maeneo mbalimbali
wanamokwenda kuhamasisha watu kujitolea damu baadhi ya watu wamekuwa wakihusisha
mpango huo na mumiani huku wengine wakitamka waziwazi kuwa wakijitolea damu
watakufa. “Tunawaelimisha sana lakini bado ni tatizo, nia yetu ni kuendelea kuhamasisha
na kwa kutoa elimu hasa vijijini ambako watu wengi bado hawajatambua umuhimu wa
kijitolea kwa maendeleo ya jamii na taifa lao,”alisema.
Afisa uhusiano huyo alisema pia baadhi ya watu hasa vijana
wamekuwa na hofu ya kujitolea damu kutokana na kitendo cha wataalamu wa mpango
wa taifa wa damu salama kupima damu kwa lengo la kujua usalama wa damu hiyo
kabla ya kuchukuliwa kwa matumizi ya watu wengine. Pamoja na ushauri unaotolewa
na wataalamu hao kabla ya kupima damu, wengi bado hawapendi kujitokeza kwa
kuhofia kupata majibu ya damu zao kuchafuka wakihusisha upimaji huo na upimaji
wa virusi vya Ukimwi (VVU).
Kutokana na kadhia hiyo, alisema imesababisha taasisi hiyo
kukusanya lita 45,000 hadi kufikia katikati ya mwezi huu sawa na asilimia 22.5
ya wastani wa malengo ya kukusanya lita 200,000 hadi mwishoni mwa mwaka huu.
“Hatuna imani ya
kufikia malengo hayo kwa muda uliobaki, ingawa mpango wetu ulikuwa kukusanya
kiasi hicho hadi Desemba mwaka huu, ”alisema, Hamadi. Anasema kundi kubwa la
wachangiaji wa damu ni watu wenye umri kati ya 36 hadi 45 kutokana na tathimini
kuonesha kuwa kundi hilo kutokuwa na hofu kwa kile kinachoelezwa kuwa wengi wao
wamepita kipindi cha hatari. Ili kukabiliana na hali hiyo, anasema mpango ni
kuongeza elimu zaidi vijijini kwa lengo la kila Mtanzania kutambua umuhimu wa
kuchangia damu kuwa ni jambo linalomhusu kutokana na ukweli kwamba kila mtu ni
mhitaji wa damu wakati wowote.
“Kila mtu mwenye afya
anapaswa kuchangia damu kwasababu asipochangia anatakiwa kujiuliza kwamba yeye
atakapopatwa na tatizo linalohitaji kuongezewa damu atachangiwa na nani?”
alihoji. Anasema mkakati mwingine ni kila hospitali ya mkoa, wilaya na rufaa kuwa
na benki ya damu kwa lengo la kuondoa hali ya kuwa tegemezi kwani kwa kipindi
kirefu hospitali hizo zimekuwa zikitegemea damu kutoka benki ya Mpango wa Taifa
wa Damu Salama makao makuu Jijini Dar es Salaam.
Mkakati huo ambao ulianza mapema mwaka huu unakwenda
sambamba na uanzishwaji wa vilabu vya damu salama kwenye shule mbalimbali nchini
kote, kutoa elimu katika taasisi za dini na kwenye vyombo vya habari vya umma
na binafsi. Takwimu za hivi karibuni zinaonesha wanawake 432 kati ya vizazi hai
100,000 hufa kila mwaka kutokana na uzazi ambapo asilimia 80 ya vifo hivyo husababishwa
na ukosefu wa damu.
Tatizo hilo pia linazipata nchi zingine zinazoendelea ambapo
nusu ya vifo hutokana na ukosefu wa damu na robo tatu hutokea Kusini mwa Asia. Katika
mkoa wa Dar es Salaam pekee, takwimu zinaonesha kuwapo kwa mahitaji makubwa ya
chupa za damu 4,000 ukilinganisha na kiasi kinachopatikana cha chupa 2,000 sawa
na nusu ya mahitaji na ongezeko la upungufu wa asilimia 70 hali ambayo
inaelezwa kuwa ni hatari. Kwa hali hyo afisa uhusiano wa mpango huo anasema ni
muhimu watu kuchangia damu kutokana na asilimia 80 ya damu inayokusanywa hutumika
kwa watoto chini ya miaka mitano, akina mama wenye matatizo ya ujauzito, uzazi
na majeruhi.
“Mtu mzima ana
wastani wa lita 5 za damu katika mwili wake. Kiasi kinachochukuliwa wakati wa
kutoa damu ni ujazo wa mililita 450, hii ni asilimia 10 tu ya damu yote
mwilini. Baada ya kujitolea damu uwingi wa damu katika mwili hurudia hali ya
kawaida ndani ya masaa 36, “alisema Hamadi.
Anataja sifa na vigezo kwa mtu anayetaka kuchangia damu kuwa
sharti awe na afya njema, uzito kuanzia kilogramu50, umri wa kati ya miaka 18
hadi 65 na kwa wanawake, asiwe mjamzito au anayenyonyeshana na kwamba mtu
anaweza kurudia kutoa damu kila baada ya miezi mitatu kwa wanaume na kila miezi
minne kwa wanawake.
Faida za kuchangia
damu kwa hiari ni pamoja na kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo, kupunguza
madini chuma mengi kupita kiasi katika damu yanayodhoofisha utendaji kazi wa
baadhi ya kuta za moyo, hurekebisha madini chuma ya ziada katika mfumo wa damu
na kuondoa nishati joto isiyo ya lazima kwenye damu ya mchangiaji kila baada ya
kuchangia damu mililita 450.
Kila wakati unapochangia
damu, mtaalamu wa tiba, daktari au muuguzi atakupima shinikizo la damu, mapigo
ya moyo na kukufanyia vipimo vingine vya magonjwa ya kuambukiza kwa damu bila
malipo, alisema. Faida zingine ni kuongeza utambuzi wa kiwango cha chembechembe
za damu katika mfumo wa uzalishaji damu, seli za damu hupungua katika mzunguko
wa damu baada ya kuchangia, hivyo uchangiaji damu huchochea uzalishaji wa seli
mpya za damu na kuchangamsha mfumo wa uzalishaji damu, alisisitiza.
Post a Comment